Utengano wa familia unaweza kuleta shinikizo la damu au kisukari
Description
Wanadamu ni viumbe ambao hukamilika wanapokuwa kwenye jamii ambapo wanaweza kuelezea hisia zao,kujihisi wanathaminiwa na wana mchango kwa wengine. Mambo hayo yanapokosa,inaweza kuwa chanzo cha matatizo ya kiafya.Na hii ni hali ambao hukuwa nao wakimbizi ambao wametenganishwa na wapendwa wao.
Katika kambi ya Kakuma iliyoko kaunti ya Turkana,kaskazini mwa Nchi ya Wakenya,tulizungumza na wakimbizi ambao walilazimika kutengana na wapendwa wao kwa sababu ya migogoro ya kifamilia,ukoo na hata vita.
Ingawa wamepata makao katika kambi ya wakimbizi bado maisha yao hayajakamilika .
Wengi wameishi kwenye hali ya upweke,huzuni na kiwewe na kupata matatizo ya kiafya yakiwemo matatizo ya afya ya akili.
Aidha kuna wale ambao wamepatwa na maradhi kama shinikizo la damu ,kisukari,ukosefu wa usingizi na chanzo ni matatizo ambayo wamekumbana nao katika kambi,ugumu wa maisha bila watu walio karibu nawe ambao unaweza kuzungumza nao na kuliwazana.
Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu,ICRC pamoja na shirika la msalaba mwekundu nchini ,KRC,katika kujaribu kukabili hali hiyo ,zinatekeleza mpango wa kujaribu kurejesha mawasiliano na uhusiano wa familia za wakimbizi.
Kwa kuwatafuta namna ambao wakimbizi hao wanaweza kuwasiliana kupitia ujumbe wa kuandikiwa au kwa njia ya simu,mashirika hayo wanasema wamefanikiwa kuwarejeshea tabasamu wachache wenye bahati na wanaendelea kuwasaka wanafamilia zaidi kila mwaka.
Matunda ya mpango huo yameonekana miongoni mwa wakimbizi wanaozungumza na jamaa zao na pia kwa wahudumu wa kujitolea wanaotangamana karibu kila siku na wakimbizi hao kwenye kambi.